RUTO AWAAGIZA WAGENI KUACHA BIASHARA NDOGO NCHINI KENYA

 

Rais wa Kenya, William Ruto, amewaagiza raia wa kigeni wanaojihusisha na biashara ndogo ndogo nchini humo kuacha shughuli hizo, akisisitiza kuwa serikali itachukua hatua za kulinda wafanyabiashara wa ndani dhidi ya ushindani usio wa haki.

Rais Ruto alitoa kauli hiyo Jumatano, Septemba 2, 2026, baada ya kukutana na wafanyabiashara wa Biashara Ndogo, Ndogo na za Kati (MSME) katika Ikulu ya Nairobi.

Katika kikao hicho, wafanyabiashara waliwasilisha malalamiko kuhusu kuongezeka kwa ushiriki wa baadhi ya raia wa kigeni katika biashara ndogo ndogo, ikiwemo uuzaji wa bidhaa kama duvet na bidhaa nyingine ambazo kwa muda mrefu zimekuwa zikitegemea wafanyabiashara wadogo wa Kenya.

Ruto alisema serikali inalenga kuhakikisha kuwa wafanyabiashara wa ndani wanapata mazingira sawa ya kufanya biashara, huku akieleza kuwa tayari kuna Muswada unaowasilishwa Bungeni unaolenga kuweka mipaka kwa raia wa kigeni kujihusisha na aina fulani za biashara nchini humo.

Rais huyo aliwataka wafanyabiashara na wadau mbalimbali kushiriki katika majadiliano ya Muswada huo kabla haujapitishwa, ili kuhakikisha kuwa mianya yote ya kisheria inayoweza kutumiwa na wageni kuingia katika biashara ndogo ndogo inafungwa.

“Tuna Muswada Bungeni kwamba kuna baadhi ya shughuli za biashara ambazo wageni hawawezi kufanya nchini Kenya. Kwa mujibu wa sheria, nataka mketi chini na wafanyabiashara waangalie kwa sababu hatujapitisha, ili tufunge mianya yote na mtu asitoke China kuja kuwa mchuuzi,” alisema Ruto.

Rais Ruto pia alisema serikali haitasubiri hadi Muswada huo upitishwe na Bunge, bali itachukua hatua za kiutawala dhidi ya raia wa kigeni ambao kwa sasa wanajihusisha na shughuli za uchuuzi na biashara nyingine ndogo ndogo zinazolenga kulindwa kwa wafanyabiashara wa ndani.

Hatua hiyo imekuja wakati serikali ya Kenya ikiendelea kutafuta namna ya kuweka uwiano kati ya kuvutia uwekezaji wa kigeni na kulinda maslahi ya wafanyabiashara wadogo na wa kati nchini humo.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Popular Items