BMT YATANGAZA UCHAGUZI WA VIONGOZI WA CHAMA CHA WOODBALL TANZANIA, FOMU ZAPATIKANA
Baraza la Michezo la Taifa (BMT) limetangaza kufanyika kwa uchaguzi wa viongozi wa Chama cha Woodball Tanzania (TWBA), huku wanachama wenye sifa wakitakiwa kuanza mchakato wa kuwania nafasi mbalimbali za uongozi.
Kwa mujibu wa taarifa ya BMT ya Septemba 3, 2026, uchaguzi huo utafanyika tarehe 4 Oktoba 2026, jijini Dar es Salaam, na utatanguliwa na usaili wa wagombea utakaofanyika tarehe 3 Oktoba 2026.
Uchaguzi huo utasimamiwa na Kamati Maalum ya Uchaguzi ya BMT, kwa mujibu wa Katiba ya TWBA. Fomu za kuomba nafasi mbalimbali za uongozi zinapatikana katika ofisi za BMT jijini Dar es Salaam au kupitia tovuti ya BMT, kuanzia Septemba 3, 2026.
Nafasi zinazotangazwa ni pamoja na Mwenyekiti, Mwenyekiti Msaidizi, Katibu Mkuu, Katibu Mkuu Msaidizi, Mweka Hazina, Wajumbe wa Kanda pamoja na wajumbe wa Kamati mbalimbali.
BMT imeeleza kuwa waombaji wanapaswa kuwa raia wa Tanzania, wenye umri usiopungua miaka 25 na elimu isiyopungua kidato cha nne. Aidha, mwombaji anatakiwa asiwe amewahi kukutwa na kosa la jinai na awe na uzoefu katika mchezo wa Woodball au shughuli zinazohusiana na uendeshaji wa michezo.
Kwa upande wa nafasi za Mwenyekiti, Makamu Mwenyekiti, Katibu, Katibu Msaidizi na Mweka Hazina, mwombaji anatakiwa kuwa na uadilifu, haiba na hadhi ya kuiwakilisha TWBA ndani na nje ya Tanzania, pamoja na kuwa na kiwango cha elimu kisichopungua Stashahada (Diploma).
Mwisho wa kuchukua na kurudisha fomu za maombi ni tarehe 30 Septemba 2026 saa 09:30 alasiri, kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na BMT.
Kwa maelezo zaidi, waombaji wanaweza kuwasiliana na BMT kupitia namba 0683 578 186 au kutembelea tovuti ya BMT.
