RIPOTI ZA MASHAMBULIZI YA IRAN DHIDI YA KAMBI ZA MAREKANI NCHINI KUWAIT

 

Kumekuwa na ripoti za mashambulizi ya makombora na ndege zisizo na rubani kutoka Iran dhidi ya kambi za kijeshi za Marekani nchini Kuwait.

Ripoti hizo zimekuja muda mfupi baada ya Jeshi la Kuwait kutangaza kuwa mifumo yake ya ulinzi wa anga iliwekwa katika hali ya tahadhari na kushiriki katika kuzuia mashambulizi ya makombora na ndege zisizo na rubani yaliyodaiwa kutoka Iran.

Takribani saa moja baada ya taarifa hiyo, shirika la habari la Tasnim, linalohusishwa kwa karibu na Walinzi wa Mapinduzi wa Iran, liliripoti kwamba kambi za Marekani nchini Kuwait zililengwa na makombora na ndege zisizo na rubani za Iran.

Hata hivyo, Tasnim haikutoa maelezo zaidi kuhusu idadi ya mashambulizi, maeneo yaliyolengwa au iwapo kulikuwa na madhara kwa watu na miundombinu.

Kwa upande wa Marekani, CENTCOM, Amri Kuu ya Jeshi la Marekani inayosimamia operesheni za kijeshi katika eneo hilo, bado haijatoa taarifa rasmi kuhusu madai hayo.

Taarifa zaidi kuhusu mashambulizi hayo zimekuwa ngumu kuthibitishwa kwa njia huru kutokana na udhibiti mkali wa upatikanaji wa taarifa katika baadhi ya nchi za Ghuba ya Uajemi, hali inayofanya iwe vigumu kwa vyombo vya habari kufika moja kwa moja katika maeneo yanayodaiwa kushambuliwa.

Aidha, vikwazo vilivyowekwa na Marekani kuhusu uchapishaji wa baadhi ya picha za setilaiti za maeneo nyeti za kijeshi vimeongeza ugumu wa kupata ushahidi wa moja kwa moja wa madhara yanayodaiwa kusababishwa na mashambulizi hayo.

Wakati huo huo, siku ya Jumatano, Tasnim ilichapisha picha za angani ilizodai kuhusishwa na mashambulizi yaliyofanywa Jumanne dhidi ya kambi za Marekani nchini Jordan.

Shirika hilo lilidai kuwa picha hizo zinaonyesha athari za mashambulizi katika maeneo yaliyolengwa, ingawa madai hayo bado yanahitaji uthibitisho huru kutoka vyanzo vingine.

Hadi sasa, taarifa kamili kuhusu ukubwa wa mashambulizi, madhara yaliyosababishwa na iwapo kulikuwa na majeruhi bado hazijathibitishwa rasmi.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Popular Items