Kama kuna jambo lililokuwa gumu kulificha katika viwanja vya Kituo cha Mafunzo ya Kijeshi Mlele jana, Agosti 29, 2026, basi halikuwa jua la Katavi wala vumbi lililokuwa likipaa uwanjani; lilikuwa fahari iliyokuwa ikionekana kwenye nyuso za askari wapya 328 wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS).
Waliposimama mbele ya viongozi, wageni na wananchi katika hafla ya kuhitimisha mafunzo yao ya awali ya kijeshi, haikuwa tena picha ya vijana waliokuja Mlele miezi sita iliyopita. Kilichoonekana ni kundi lililojaa morali, nidhamu, ujasiri na kujiamini! Kundi ambalo tayari lilionekana kuelewa kuwa kazi iliyokuwa mbele yao haikuwa kulinda misitu pekee, bali kulinda sehemu muhimu ya maisha ya Taifa.
Na hapo ndipo kauli ya “TFS ni Bonge la Taasisi” ilipopata maana ya kipekee. Kauli hiyo si maneno yaliyobuniwa siku ya hafla; ni slogan inayotumiwa na TFS kuonyesha fahari ya watumishi wake kwa taasisi yao. Siku hiyo, wahitimu waliibeba slogan hiyo kupitia kwaya yao, wakiimba kwa kujiamini na kuonyesha kwa vitendo fahari yao ya kuwa sehemu ya TFS. Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt. Ashatu Kijaji, naye akaipokea na kuithibitisha mbele ya hadhara, akipongeza Bodi na Menejimenti ya TFS na kukiri kuwa vijana hao “wameiva”, huku akitoa pongezi kwa Bodi na Menejimenti ya TFS chini ya Kamishna wa Uhifadhi, Prof. Dos Santos Silayo.
Kutoka kwenye slogan hadi ushahidi wa uwanjani
Kauli hiyo ya Waziri haikuzaliwa hewani. Iliungwa mkono na miezi sita ya mafunzo yaliyolenga kubadilisha kabisa namna askari hao wapya wanavyoutazama utumishi wao.
Mafunzo hayo hayakuishia kwenye gwaride, sare na mazoezi ya kijeshi. Askari walifundishwa mbinu za doria na ufuatiliaji, utunzaji wa mazingira, sheria za misitu na wanyamapori, huduma kwa watalii, huduma ya kwanza, usalama, uchunguzi wa awali wa makosa, usimamizi wa migogoro, matumizi sahihi ya nguvu, haki za binadamu na masuala ya utekelezaji wa sheria. Mafunzo hayo yalihusisha pia ushirikiano wa wakufunzi kutoka Jeshi la Uhifadhi, Polisi, JWTZ na Ofisi ya Usalama wa Taifa.
Kwa maana nyingine, TFS haikuwa ikitengeneza askari wa kukimbiza wahalifu pekee; ilikuwa ikitengeneza mtumishi wa uhifadhi mwenye uwezo wa kukabiliana na mazingira halisi ya kazi.
Na hapa ndipo ukubwa wa taasisi hii unapoanza kuonekana.
Askari 328, lakini dhamana ni ya taifa zima
Askari wote 328 walioanza mafunzo hayo walimaliz, jambo ambalo Waziri Kijaji alilitaja kama jambo la kujivunia, akiwakumbusha kuwa miezi sita waliyomaliza ni mwanzo tu wa safari yao ya utumishi.
Lakini nyuma ya idadi hiyo kuna jambo kubwa zaidi.
Misitu inayosimamiwa na TFS si mkusanyiko wa miti tu. Kwa mujibu wa Waziri, misitu ni sehemu ya maisha ya Watanzania; inatunza mazingira, vyanzo vya maji, ardhi na maisha ya jamii na wanyamapori. Hivyo, anaposema vijana hao wameiva, maana yake ni kwamba Taifa limeongeza nguvu katika kulinda mfumo mzima wa maisha unaotegemea rasilimali hizo.
Ndiyo maana Kamishna wa Uhifadhi wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) Prof. Silayo akasisitiza kuwa ajira za vijana hao zimeongeza nguvu kazi katika uhifadhi, hasa katika maeneo ambayo askari hao watapangiwa kufanya kazi.
Mhe. Dkt. Kijaji hakutaka vijana hao waondoke Mlele wakiamini wamefika mwisho. Badala yake, aliwaita wahitimu wa “kindergarten”, akimaanisha kuwa mafunzo halisi ya utumishi ndiyo yanaanza sasa.
Aliwataka watunze nidhamu, walinde siri za kazi na Taifa, walinde rasilimali kwa uadilifu na ujasiri, waheshimu sheria, mamlaka na wananchi, na wafanye kazi kwa uzalendo bila kuogopa changamoto.
Hapo ndipo “bonge la taasisi” linapopimwa! Si kwa idadi ya askari wanaovaa sare, bali kwa aina ya mtumishi anayezalishwa na taasisi hiyo.
TFS mpya: Jeshi linalotakiwa kuwa rafiki wa wananchi
Huenda sehemu iliyobeba ujumbe mkubwa zaidi katika hotuba ya Waziri ilikuwa pale alipowataka askari hao kubadilisha taswira ya Jeshi la Uhifadhi kwa wananchi.
Badala ya mwananchi kumuona askari kama adui, Waziri anataka askari awe mshirika wa mwananchi katika kulinda misitu. Ndiyo maana alipendekeza hata wimbo wa Jeshi la Uhifadhi ufundishwe katika shule za msingi zinazozunguka maeneo ya hifadhi ili watoto waanze mapema kuelewa kuwa bila misitu hakuna maisha.
Hii ni fikra inayokwenda mbali zaidi ya doria.
Ni fikra ya kujenga kizazi ambacho hakilindi msitu kwa sababu kinaogopa askari, bali kwa sababu kinaelewa thamani yake.
Mlele yenyewe nayo inabadilika
Na inaonekana Serikali nayo imeamua kuwa kama TFS na taasisi zingine zinazounda Jeshi la Uhifadhi zinataka kuwa taasisi kubwa zaidi, basi mahali pa kuwajenga watumishi wake lazima paende sambamba na dhamana hiyo.
Waziri alitangaza kuwa Serikali imetenga Sh bilioni 4.354 katika mwaka wa fedha 2026/27 kwa ajili ya kuboresha miundombinu ya Kituo cha Mafunzo ya Kijeshi Mlele. Maboresho hayo yanahusisha maeneo ya malazi, madarasa, maeneo ya mafunzo, jiko na miundombinu mingine.
Zaidi ya hapo, Mlele inatarajiwa kubadilika kutoka kituo cha mafunzo kuwa chuo cha mafunzo ya Jeshi la Uhifadhi kitakachofanya kazi mwaka mzima na kutoa mafunzo endelevu kwa viwango vya kitaifa na kimataifa.
Na kuna jambo jingine la kuvutia: mtaala nao unapanuliwa, ukiwemo uokoaji majini, huku Serikali ikiridhia kujengwa kwa bwawa la kuogelea lenye ukubwa wa mashindano ya Olimpiki kwa ajili ya mafunzo hayo.
Challenge ya Waziri kwa Makamishna
Mwisho wa siku, Mlele haikuwa sherehe ya askari 328 pekee. Ilikuwa kama kioo kilichowekwa mbele ya taasisi za uhifadhi.
Waziri Kijaji aliwaona vijana hao wakijivunia kuwa sehemu ya TFS na akawataka waende kazini na kuionesha fahari hiyo kwa vitendo, hadi misitu na wananchi wanaowazunguka watambue kuwa kuna vijana waliodhamiria kuilinda taasisi, rasilimali na Taifa.
Lakini Waziri akaweka challenge kwa makamishna wengine wa taasisi za uhifadhi: fahari ya taasisi haipaswi kubaki kwenye maneno, nyimbo au sare; lazima ionekane katika matokeo ya kazi na namna taasisi inavyowajenga watumishi wake.
Kwa maana hiyo, Mlele ilikuwa na ‘vibe lakutosha’. TFS ilikuwa inaonyesha kile inachoweza kufanya, na sasa taasisi nyingine za uhifadhi zinaalikwa kuonyesha uwezo wao kwa vitendo.Huo ndio uzito wa challenge ya Waziri: TFS imeweka kiwango; sasa imebaki kwa wengine kuonyeshe wanaweza kufikia au kuvuka kiwango hicho.
Mwisho wa siku, Mlele haikuandika tu ukurasa mpya wa wahitimu 328; iliandika ukurasa mpya wa matarajio ya Taifa kwa Jeshi la Uhifadhi. Wakati kwaya ya wahitimu ikiimba kwa fahari “TFS ni Bonge la Taasisi”, kauli hiyo haikusalia kwenye jukwaa la hafla, ilibeba ahadi ya kizazi kipya cha walinzi wa rasilimali za Taifa.

.jpg)
