RAIS MWINYI AWASILI BELGRADE KUMWAKILISHA RAIS SAMIA KWENYE MAADHIMISHO YA MIAKA 65 YA HARAKATI YA NCHI ZISIZOFUNGAMANA






 Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi, amewasili mjini Belgrade, Serbia, kwa ajili ya kuiwakilisha Tanzania katika mkutano wa ngazi ya juu wa kuadhimisha miaka 65 tangu kuanzishwa kwa Harakati ya Nchi Zisizofungamana (Non-Aligned Movement – NAM).

Dkt. Mwinyi anaiwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, katika maadhimisho hayo yanayofanyika nchini Serbia.

Baada ya kuwasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Nikola Tesla, Rais Mwinyi alipokelewa rasmi na Naibu Waziri Mkuu wa Serbia ambaye pia ni Waziri wa Uchumi, Andrijana Mesarović, hatua iliyoashiria kuanza kwa ratiba yake rasmi ya kikazi nchini humo.

Mkutano huo wa ngazi ya juu umepangwa kufanyika Agosti 31 hadi Septemba 1, 2026, katika Ikulu ya Serbia, Belgrade. Mkutano huo unalenga kuadhimisha miaka 65 tangu kufanyika kwa Mkutano wa Kwanza wa Harakati ya Nchi Zisizofungamana, uliofanyika Belgrade mwaka 1961.

Katika maadhimisho hayo, mataifa mbalimbali yanatarajiwa kutafakari mchango wa Harakati ya Nchi Zisizofungamana katika masuala ya kimataifa pamoja na umuhimu wa misingi yake katika kukabiliana na changamoto za kisiasa, kiuchumi na kiusalama zinazolikabili dunia kwa sasa.

Rais Mwinyi anashiriki maadhimisho hayo kwa niaba ya Rais Samia na anatarajiwa kuwasilisha tamko la kitaifa la Tanzania katika mkutano huo wa ngazi ya juu.




Post a Comment

Previous Post Next Post

Popular Items