Kampuni ya usafiri wa abiria mtandaoni, Uber, imetangaza kusitisha mara moja shughuli zake nchini Nigeria na Uganda, baada ya kufanya tathmini ya kina ya shughuli zake za kibiashara katika masoko hayo.
Uber, ambayo ni miongoni mwa kampuni kubwa duniani katika huduma za usafiri kupitia programu za simu, imesema imefikia “uamuzi mgumu” wa kuondoka katika nchi hizo mbili za Afrika.
Kampuni hiyo ilianza kutoa huduma nchini Nigeria mwaka 2014, kabla ya kuingia katika soko la Uganda mwaka 2016.
Nchini Nigeria, madereva wanaofanya kazi kupitia Uber wamekuwa wakilalamikia kwa muda mrefu viwango vya nauli vinavyowekwa kupitia programu hiyo, wakisema havijaendana na ongezeko la gharama za uendeshaji, hususan kupanda kwa bei ya mafuta.
Madereva pia wamekuwa wakieleza kutoridhishwa na kiwango cha kamisheni kinachokatwa na kampuni, wakidai kuwa kinapunguza mapato yao.
Mbali na changamoto hizo, Uber imekuwa ikikabiliwa na ushindani kutoka kwa majukwaa mengine ya usafiri yanayotoa huduma zinazofanana katika masoko hayo.
Tangazo la kuondoka Nigeria na Uganda limekuja wakati kampuni hiyo pia ikikabiliwa na mabadiliko katika shughuli zake duniani.
Mkurugenzi Mtendaji wa Uber, Dara Khosrowshahi, ameeleza kuwa kampuni hiyo inapanga kupunguza takribani asilimia 10 ya wafanyakazi wake duniani, ikiwa ni sehemu ya hatua za kupunguza gharama na kuimarisha ufanisi wa kampuni.
Uamuzi wa Uber kuondoka katika masoko hayo mawili unatarajiwa kuwa na athari kwa maelfu ya madereva na abiria waliokuwa wakitegemea huduma hiyo, huku ukifungua nafasi kwa kampuni nyingine za usafiri wa kidijitali kuongeza ushindani katika masoko ya Afrika.
Tags:
International News
