Katika kikao hicho, Kamati ya Miundombinu iliwasilisha taarifa kuhusu maendeleo ya maboresho ya Uwanja wa Benjamin Mkapa, ujenzi wa Uwanja wa Arusha pamoja na Uwanja wa Fumba Zanzibar. Aidha, taarifa hiyo ilihusu maboresho na ujenzi wa viwanja vya mazoezi vitakavyotumika wakati wa mashindano hayo.
Kwa upande mwingine, Kamati ya Sheria na Masoko iliwasilisha mipango na mikakati ya kuhakikisha Tanzania inanufaika na AFCON 2027 katika nyanja mbalimbali, ikiwemo kutangaza na kuendeleza vivutio vya utalii vinavyopatikana Tanzania na Zanzibar, hivyo kutumia mashindano hayo kama fursa ya kuitangaza nchi kimataifa.
Akizungumza katika kikao hicho, Mwenyekiti wa Kamati ya Ndani ya Kuratibu na Kusimamia Mashindano ya AFCON 2027, Bw. Leodgar Tenga, amewahimiza wajumbe wa kamati mbalimbali kuhakikisha kila mmoja anatimiza wajibu wake ipasavyo ili mashindano hayo yawe na manufaa makubwa kwa Taifa.AFCON 2027 inatarajiwa kufanyika kuanzia Juni 19 hadi Julai 17, 2027, huku Tanzania, Kenya na Uganda zikiwa wenyeji wa mashindano hayo. Maandalizi hayo hayalengi kuhakikisha michuano inafanyika kwa mafanikio pekee, bali pia kutumia AFCON 2027 kama fursa adhimu ya kuchochea ajira, kuongeza pato la Taifa, kukuza sekta ya utalii na kuimarisha miundombinu ya kisasa, ikiwemo ya michezo, barabara na viwanja vya ndege.
Kikao hicho ni sehemu ya hatua endelevu za Tanzania katika kuratibu, kusimamia na kuimarisha maandalizi kuelekea AFCON 2027, huku msisitizo ukiwekwa katika kuhakikisha urithi wa mashindano hayo unaendelea kuwa na manufaa kwa Watanzania hata baada ya mashindano kumalizika



.jpeg)