Na Mussa Augustine:Dar es Salaam
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Deogratius Ndejembi, anatarajiwa kuwa Mgeni Rasmi katika Kongamano la Tano la Kimataifa la Uchumi wa Buluu, litakalofanyika Septemba 7 hadi 9, mwaka huu katika Ukumbi wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNICC), jijini Dar es Salaam.
Kongamano hilo linatarajiwa kuwa jukwaa muhimu kwa wataalamu, watafiti, watunga sera na wadau mbalimbali kujadili fursa zinazotokana na rasilimali za bahari na maji, huku vijana wakipewa nafasi ya kujifunza na kutambua fursa za kiuchumi zilizopo katika sekta hiyo.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam mapema leo,Mkuu wa Chuo cha Bahari Dar es Salaam, Tumaini Gurumo, alisema kongamano hilo litawakutanisha washiriki kutoka Tanzania, Afrika na mataifa mbalimbali duniani.
Alisema pia kutakuwa na mawasilisho ya kitaalamu pamoja na uwasilishaji wa matokeo ya tafiti mbalimbali zilizofanywa na wanasayansi na watafiti katika maeneo tofauti ya Uchumi wa Buluu.
Kwa mujibu wa Gurumo, tafiti hizo zitajadiliwa kwa lengo la kubaini changamoto zinazoikabili sekta hiyo, kutafuta suluhisho na kuweka mikakati ya kutumia matokeo ya tafiti hizo katika kukuza Uchumi wa Buluu nchini na barani Afrika.
VIJANA KUPATA FURSA
Gurumo alisema vijana kutoka vyuo vikuu, shule za sekondari na shule za msingi wamealikwa kushiriki katika kongamano hilo ili kuwajengea uelewa kuhusu fursa zinazopatikana katika Uchumi wa Buluu.
Alisema hatua hiyo inalenga kuhakikisha vijana wanaifahamu sekta hiyo mapema na kutambua nafasi waliyonayo katika kuitumia rasilimali za maji kwa ajili ya kujiajiri, kuajiriwa na kuanzisha shughuli za kiuchumi.
“Ni muhimu vijana wetu wakaifahamu agenda ya Uchumi wa Buluu wakiwa bado katika umri mdogo, kwa sababu wao ndio watakaobeba jukumu la kuendeleza sekta hii katika siku zijazo,” alisema.
WASHIRIKI KUTOKA NCHI MBALIMBALI
Kongamano hilo linatarajiwa kushirikisha washiriki kutoka ndani na nje ya Tanzania, wakiwamo kutoka Kenya, Ghana, Afrika Kusini, Comoro, Seychelles na Uganda.
Nchi nyingine nje ya Afrika zinazotarajiwa kushiriki ni Japan, Sweden na Urusi, huku mabalozi wanaowakilisha mataifa mbalimbali nchini Tanzania, viongozi wa taasisi za serikali na binafsi, wanasayansi, watafiti, watunga sera na wadau wa Uchumi wa Buluu wakitarajiwa kuhudhuria.
Gurumo alisema kongamano hilo pia linaendana na Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 pamoja na Ajenda 2063 ya Umoja wa Afrika, ambazo zinasisitiza matumizi endelevu ya rasilimali kwa ajili ya maendeleo ya kiuchumi na kijamii.Alisema Tanzania ina fursa kubwa kupitia bahari, mito, maziwa na rasilimali nyingine za maji, hivyo ni muhimu kwa wadau kushirikiana katika kuzitumia kwa njia endelevu na kuongeza mchango wake katika uchumi wa taifa.

