Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji ameielekeza Kamati ya Tathmini ya kuanzishwa kwa Jumuiya mpya ya Hifadhi ya Wanyamapori Ziwa Natron kuhakikisha inafanya utafiti wa kina huku ikijikita zaidi katika kuwasikiliza wananchi wanataka nini lakini pia kuwaelimisha juu ya sheria, kanuni na taratibu ili maamuzi sahihi yaweze kufanyika kwa manufaa ya wananchi na kudumisha uhifadhi.
Waziri Kijaji amesema hayo Agosti 31, 2026 wakati akipokea taarifa ya tathmini ya maombi ya Halmashauri ya Wilaya ya Longido ya kuanzishwa kwa Jumuiya ya Hifadhi ya Wanyamapori Ziwa Natron pamoja na kuunganishwa kwa malipo ya wanufaika.
Katika kikao hicho kilichofanyika katika ukumbi wa Chuo cha Taifa cha Utalii (NCT) Jijini Dar es Salaam, Waziri Kijaji ameisisitiza kamati kusikiliza maoni na mahitaji ya wananchi kama sehemu ya kuihusisha jamii katika jukumu la uhifadhi lakini pia kuhakikisha jamii inapatiwa elimu ya kutosha juu ya mambo yanayotakiwa na yasiyotakiwa kufanyika ili maamuzi yatakayofanyika yawe yamezingatia ushirikishwaji wa kila kundi linaloguswa.
Tags:
Local News



